Ticker

6/recent/ticker-posts

AGENDA ,NEMC YAWAKUTANISHA WADAU KUWEKA MKAKATI KUDHIBITI TAKA HATARISHI ZINAZOTOKANA NA BETRI CHAKAVU

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

WADAU mbalimbali wakiwemo Asasi isiyo ya kiserikali ya AGENDA pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wamekutana katika warsha maalumu kwa lengo la kujadili na kuangalia namna bora ya usimamizi wa taka hatarishi zinazotokana na betri chakavu.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na AGENDA kwa kushirikiana na NEMC pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Oeko-Institut ya Ujerumani kwa ufadhili wa Shirika la ushirikiano wa kimataifa la Ujerumani (GIZ) wadau wametoa sababu mbalimbali za msingi kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa mkakati wa kudhibiti taka hizo hatarishi zinazotokana na uwepo wa betri chakavu.

Akizungumza leo Oktoba 21,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa warsha hiyo, Meneja wa Uzingatiaji wa NEMC, Hamad Taimuru, ayemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema lengo la warsha hiyo ni kutoa mwongozo bora kuhusu usimamizi wa betri chakavu ili kuepusha madhara kwa mazingira na afya ya jamii.

Ametumia warsha hiyo kutoa rai kwa wamiliki wa viwanda vinavyojihusisha na urejelezaji wa betri chakavu kuhakikisha wanatekeleza Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kuanza shughuli hizo.

Pia amewakumbusha umuhimu wa kupata vibali maalum kutoka NEMC na taasisi nyingine za Serikali kwa ajili ya kuhakikisha mchakato wa urejelezaji unazingatia sheria, kanuni, na taratibu za mazingira.

"Ni matarajio yetu kwamba warsha hii itatoa uelekeo mzuri wa namna bora ya usimamizi wa taka hatarishi ili zisilete madhara kwa afya ya binadamu na mazingira,” amesema na kufafanua hii ni wiki ya kuchukua tahadhari dhidi ya uchafuzi unaotokana na betri chakavu.

Wakati huo huo Katibu Mtendaji wa Taasisi ya AGENDA, Dora Swai, amesema kuwa urejelezaji wa betri chakavu ni hatari endapo hautasimamiwa ipasavyo.

Amesema kwamba madini yanayopatikana kwenye betri chakavu, hususan ‘lead,’ yana madhara makubwa kwa mazingira na afya ya binadamu, na yanaweza kusababisha magonjwa ya figo, ini, na ubongo.

Kwa upande wake Mratibu wa Shughuli za Taasisi ya Wadau wa Urejelezaji Tanzania (TARA), Henry Kazula, amewaomba wadau wote kuongeza uelewa kuhusu urejelezaji wa taka hatarishi.

Wadau wengine walioshiriki katika warsha hiyo ni maofisa mazingira wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, OSHA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na wamiliki wa viwanda vinavyohusika na urejelezaji wa taka hatarishi.


Post a Comment

0 Comments