NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Dkt. Godwin Lekundayo, amewataka wahitimu wa mafunzo ya sanaa ya muziki kuwa walimu na kielelezo bora katika makanisa yao.
Kauli hiyo ameitoa leo, Oktoba 5, 2024, kwenye Mahafali ya awamu ya 13 ya Mafunzo ya sanaa ya muziki kwa Waadventista Wasabato katika Chuo Cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)
Dkt. Lekundayo amesisitiza umuhimu wa muziki katika maisha ya waumini na jamii kwa ujumla, akiwataka wahitimu kutenda kwa mfano mzuri na kuwafundisha wengine kuhusu umuhimu wa sanaa.
Aidha, aliwasisitiza waumini kujitokeza kupiga kura kwa njia halali ili kuimarisha imani yao kwa serikali.
Mkufunzi wa Muziki TASUBA, Heri Kaare, amesema kuwa wahitimu 65 wa kanisa hilo wamefanikiwa kumaliza mafunzo hayo, ambayo yamefanyika kwa awamu ya 13 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.
Kaare ameongeza kuwa muziki ni muhimu katika nyanja zote za maisha, akisisitiza kwamba unahitajika katika siasa, ibada, misiba, na sherehe.
Pamoja na hayo, Mwalimu Kaare ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa awamu tatu, ambapo wanafunzi wanaweza kurudi kwa ajili ya kuimarisha ujuzi wao.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Bw. Emmanuel Bwire, ametoa rai kwa wahitimu kuwa mabalozi wa TASUBA na kuwafundisha wengine, huku Sista Pietra Nicholaus kutoka Shirika la Huruma ya Mungu, Jimbo la Tanga, akipongeza mafunzo hayo, akieleza jinsi alivyoweza kujifunza kuimba, kusoma nota, na kupiga kinanda.
0 Comments