Na: Fortunatus Charles Kasomfi, Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, ameipongeza Jumuiya ya maendeleo nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kwa hatua muhimu iliyofikiwa katika kumairishwa kwa Demokrasia, Amani, Ulinzi, Usalama na Maendeleo kwa Nchi za Jumuiya hiyo.
Akiungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuwasili Jijini Gaborone Nchini Botswana, kutekeleza majukumu ya uangalizi wa uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Botswana akiwa mwangalizi mkuu kutoka SADC, Mhe. Pinda amesema kuimarishwa kwa Demokrasia, Amani na Utulivu ni hatua mahimu katika kuleta Maendeleo ya Nchi yeyote ile Duniani.
“ Mpango wa kuangalia na kuwezesha chaguzi zenye utulivu kwa raia wa Kanda ya SADC na kupata viongozi wawatakao ni jambo jema sana na katika hili ninaipongeza sana Jumuiya na pia ninavipongeza na kuvishukuru Vyombo mbalimbali vya Habari vinavyofanya kazi nzuri ya kuhabarisha na kuelimisha umma Duniani kote kuhusu hatua muhimu za utekelezwaji wa michakato ya Kidemokrasia zinavyofanyika ukiwemo uchaguzi Mkuu wa Botswana”. Amesema Mhe. Pinda.
Mhe. Pinda aliteuliwa kuongoza Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Troika) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Pinda atazindua rasmi Misheni ya SEOM inayoundwa na wajumbe kutoka Nchi Wanachama wa SADC tarehe 22 Oktoba, 2024 na pia kwa kushirikiana na Wajumbe wengine wa Troika (Zambia na Malawi) atakutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Botswana, Vyama vya siasa, Asasi za Kiraia, Taasisi za dini na Vyombo vya Habari kwa ajili ya kuelezea kazi ambayo SEOM itafanya katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu hadi kukamilika kwake.
Mhe. Pinda amepokelewa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama Jijini Gaborone, Botswana na Balozi wa Tanzania nchini humo mwenye makazi yake Afrika Kusini Mhe. James Bwana.
Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Botswana utafanyika tarehe 30 Oktoba, 2024 ambapo Rais wa sasa Mhe. Mokgweetsi Masisi atawania muhula wa pili na wa mwisho baada ya chama chake tawala kuidhinisha azma yake ya kugombea kiti cha urais.
0 Comments