Ticker

6/recent/ticker-posts

VETA Yazindua Kampeni ya "VETA na Fundi Mahiri" Kuboresha Ujuzi wa Vitendo kwa Wanafunzi wa Ufundi Stadi

Katika jitihada za kuboresha ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi wa ufundi stadi, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imezindua kampeni ijulikanayo kama "VETA na Fundi Mahiri," ikilenga kuwashirikisha mafundi wabobevu (Fundi Mahiri) katika kuwaongoza na kuwapa mafunzo ya vitendo wanafunzi wa ufundi stadi, ili waweze kupata umahiri stahiki katika fani zao.

Makubaliano ya ushirikiano yalioshuhudiwa jana, tarehe 1 Oktoba 2024 kati ya Chuo Ufundi Stadi na Huduma Mkoa wa Iringa na kampuni mbili katika Manispaa ya Iringa yanaashiria mwanzo wa ushirikiano kati ya VETA na mafundi mahiri katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Mkoa wa Iringa, Bw. Pasien Nyoni, ametia saini makubaliano ya ushirikiano na mafundi mahiri Bw. Mohamed Anuarsadat, mtaalam wa magari kutoka kampuni ya TAWAQAL, David Charles Kalinga anayemiliki karakana ya Ukerezaji Vyuma (Fitter Mechanics) na kushuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore.

Akizungumza baada ya utaji Saini makubaliano hayo, CPA Kasore ameelezea umuhimu wa mpango huo, akisema, "Ushirikiano huu ni mkakati wa VETA kuziba pengo kati ya ujuzi na maarifa unaotolewa kwenye vyuo vyetu na ujuzi wa vitendo katika sehemu za kazi. Ushiriki wa mafundi mahiri utawawezesha wanafunzi wetu kupata uzoefu wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu waliobobea, kujifunza siyo tu mambo ya kiufundi, bali pia utamaduni wa sehemu za kazi na maadili muhimu kwa mafanikio yao.

Amesema mpango huo hautawafaidisha tu wanafunzi wa VETA, bali pia utasaidia kujenga nguvu kazi yenye uwezo na ujasiri inayoendana na mahitaji ya viwanda.

CPA Kasore aliongeza kuwa VETA iliamua kuanzisha mpango huo wa "VETA na Fundi Mahiri" kutokana na haja ya kushughulikia pengo la ujuzi linalowakabili vijana wengi wanaohitimu.

"Vijana wetu wengi wanayo maarifa ujuzi walioupata katika mafunzo, lakini wanahitaji kunolewa kwa mafunzo zaidi ya mahala pa kazi ili kuwaongezea umahiri wa kushindana katika soko la ajira. Kwa kushirikiana na mafundi wenye uzoefu, tunahakikisha kuwa wanafunzi wetu wanapata uongozi na mafunzo ya vitendo wanayohitaji ili kufanikiwa katika fani zao," amesema.

Akifafanua zaidi, Kasore amesema mbali na ushirikiano wa Iringa, VETA ina mpango ya kuanzisha programu ya "VETA na Fundi Mahiri" katika vyuo vingine vya ufundi stadi vinavyomilikiwa na VETA nchini kote kwa lengo la kuunda mtandao endelevu wa wataalamu ambao watawaongoza na kuwasaidia wanafunzi, na hivyo kuboresha mafunzo ya ufundi stadi.

Kwa upande wao, mafundi mahiri nao wameonesha shauku yao kwa ushirikiano huo ambapo Bw. Mohamed Anuarsadat, mtaalam wa magari mwenye uzoefu wa miaka mingi, ameelezea umuhimu wa kulea vipaji vya vijana.

"Nimefurahi kuwa sehemu ya mpango huu. Vijana hawa ndio mustakabali wa sekta yetu, na ni jukumu letu kuwapa ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kufanikiwa. Natarajia kufanya kazi nao na kuwaona wakikua na kuwa wataalamu wenye uwezo," amesema.

Naye David Charles Kalinga ameunga mkono kwa kusema, "Mpango huu hautawasaidia tu wanafunzi, bali pia utaboresha ubora wa nguvu kazi katika jamii yetu. Kwa kushirikisha utaalamu wetu, tunachangia kukuza wataalamu wenye ujuzi watakaosaidia kuendeleza sekta zetu," amesema.

Mpango huo unatarajiwa kuboresha mazingira ya mafunzo kwa kuwapatia wanafunzi wa VETA uzoefu wa hali halisi ya utendaji katika fani zao na kujifunza kutoka kwa wataalam wabobevu wa fani husika.

Mpango huu ni sehemu ya mkakati mpana wa VETA wa kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi nchini kote, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata ujuzi unaohitajika kwa ajira na ujasiriamali.

Post a Comment

0 Comments