Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WAASWA KUZINGATIA UBORA

Wazalishaji wa vyakula vya Mifugo nchini wameaswa kuzingatia ubora wanapozalisha vyakula vya Mifugo ili kulinda afya za watumiaji wa mazao yatokanayo na Mifugo, kuongeza ustawi wa Mifugo, kuongezeka kwa uzalishaji Mifugo pamoja na kukuza vipato vya wafugaji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Furaha Kabuje Oktoba 04, 2024 alipokuwa akifanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo kwa Wilaya za Mkoa wa Dar Es Salaam (Ubungo, Temeke, kigamboni na Ilala) kuanzia oktoba 1 hadi 4, 2024 kwa lengo la kufuatilia na kujiridhisha uzalishwaji wa vyakula hivyo kama vinafuata taratibu zilizowekwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

“Tunafanya ukaguzi huu kuangalia uzalishaji, kuona kazi zinazofanyika, kukagua vibali vya uzalishaji sambamba na kujiridhisha vyakula mnavyozalisha kama vimehakikiwa ubora na Maabara kuu ya Veterinari kwa lengo la kulinda afya za watumiaji wa mazao ya Mifugo.”

“Tunachukua sampuli za vyakula kwa wazalishaji pamoja na wauzaji tunakwenda kuzipima Maabara Kuu ya Veterinari. Kwa wale watakaobainika kufanya udanganyifu kwa kuzalisha vyakula visivyokidhi ubora tutawachukulia hatu kali kwa mujibu wa sheria.” Alisema Bw. Kabuje

Mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha uzalishaji wa chakula cha Mifugo cha HUATANG INVESTIMENT GROUP kilichopo Chanika Bi. Chen Meng Yan alisema kuwa kipaumbele chake kikubwa ni ubora wa chakula cha Mifugo na mara zote amekuwa akihakikisha chakula kinapimwa ubora kabla hakijakwenda sokoni ili kujihakikishia ubora.

“Hatuwezi kuzalisha chakula chenye kiwango cha chini maana kampuni yetu itakufa na hata wafanyanyakazi wetu watapoteza kazi zao, vilevile hatutaki kupata hasara ndio maana tunazingatia ubora.” Alisema Bi. Chen

Bw. Adili Krisoston muuzaji wa vyakula vya Mifugo ameishukuru Serikali kwa kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo mara kwa mara kwani kitendo hicho kinawahakikishia kuwa vyakula wanavyovinunua kwa wazalishaji vinakaguliwa na vinakidhi ubora kwa ustawi wa Mifugo pamoja na afya za watumiaji wa mazao ya Mifugo.
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Furaha Kabuje (kulia) akichunguza sampuli ya vyakula vya Mifugo pamoja na timu ya ukaguzi aliyoongozana nayo kwenye kiwanda cha uzalishaji wa vyakula hivyo cha HUATANG INVESTIMENT GROUP alipokwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo kwa wasindikaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo Oktoba 04, 2024 Chanika Wilaya ya Ilala Dar Es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Furaha Kabuje (mwenye miwani) akichukua sampuli ya vyakula vya Mifugo kutoka kwa muuzaji wa vyakula hivyo Bw. Adili Krisoston kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi kama vinakizi viwango vya ubora Oktoba 04, 2024 alipokwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo kwa wasindikaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo Chanika Wilaya ya Ilala Dar Es Salaam. Wa pili kutoka kulia ni mmiliki wa kiwanda hicho Bi. Chen Meng Yan
Meneja wa Maabara Kuu ya Veterinari wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Geofrey Omarch (kulia) akichukua sampuli ya vyakula vya Mifugo kutoka kwa muuzaji wa vyakula hivyo kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi kama vinakizi viwango vya ubora Oktoba 01, 2024 alipokwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo kwa wasindikaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo Ubungo Dar Es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyama wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Scholastika Dotto akikagua sampuli ya vyakula vya Mifugo kwenye kiwanda cha kuzalisha chakula cha Mifugo (One one Animal Feed kilichopo Chamanzi Temeke Dar Es Salaam Oktoba 02, 2024 alipokwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo kwa wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo. Kulia kwake ni Msimamizi wa kiwanda hicho Bw. Festo Mkapa

Post a Comment

0 Comments