NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Nangi Massawe amesema mfumo wa kidigitali wa utatuzi wa Malalamiko kuhusu huduma za kifedha kwa wananchi umekamilika na unakwenda kurahisisha kutatua changamoto kwa haraka.
Ameyasema hayo leo Desemba 10, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku mbili kuhusu mfumo wa malalamiko kwa watoa huduma za kifedha kuhusu mfumo wa malalamiko utakavyofanya kazi.
Aidha Nangi amesema jukumu kubwa la benki kuu ni kuhakikisha linamlinda mtumiaji wa huduma za kifedha kuwa na uelewa wa masuala ya kifedha, kujua ni wapi atawasilisha malalamiko yake na kupata haki.
"Mfumo wa malalamiko umetengenezwa na kukamilika, tunaamini ifikapo Januari tutauzindua rasmi wananchi waweze kutuma malalamiko yao, ni muhimu sana kuulewa kupitia warsha hii, kwa sababu tutahakikisha kama kuna tatizo mteja anafikisha kwa haraka na linafika kwa haraka na kupata haki yake kwa haraka," Amesema Nangi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha, Dkt. Khadija Kishimba amewataka watumie mfumo huo kwa sababu unakwenda kusogeza huduma kwa mwananchi kwani wanataka alalamike kupitia mtandao kwa njia ya kompyuta.
Amesema kwa sasa wanapokea malalamiko kupitia matawi yao na dawati ya malamiko kupitia njia ya barua pepe, simu au kuandika barua na kufikisha hivyo, waona njia hiyo inaweza kutowafikisha zaidi ya teknolojia.
Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Elizabeth Mhina amesema kupitia mfumo huo wa kidigitali utawasaidia kurahisisha kazi na kuwafikia wateja na Watanzania kwa ujumla kwa urahisi na kwa haraka.
"Kuna malalamiko mengi tumekuwa tukiyapokea, kikubwa ni changamoto ya elimu kwa wateja, kwa mfano kuibiwa fedha katika ATM na ndo maana tumekuwa tukiwasihi wateja wetu kulinda namba zao za siri na wasimuamini mtu yoyote kumtajia namba ya siri". Amesema
Hata hivyo kwa upande wake mtoa huduma za fedha wa benki ya CRDB, Lugano Mponjoli amesema hatua hiyo italeta mabadiliko katika mfumo wa fedha na kutatua changamoto za wateja kwa muda mfupi ikiwemo za kuibiwa fedha.
0 Comments