Mgeni rasmi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Augustine Masesa akikabidhiwa Kitabu Usiishie Njiani na Mwandishi wa Kitabu hicho Eng. Avith Amos.
Na Mtemi Sona
Hifadhi ya Mikumi iligeuka kituo cha kipekee cha uzinduzi wa kitabu "Usiishie Njiani" kilichoandikwa na Mhandisi Avith Amos Kandubuka, Jumamosi, Novemba 30, 2024. Tukio hilo lilifanyika usiku, likihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa taasisi za serikali, wadau wa utalii (Shangwe Tour) na wadau wengine wa sekta mbalimbali.
Kitabu hicho, ambacho kinaangazia mbinu za kumwezesha mtu kutimiza malengo yake, ni msaada wa kipekee kwa yeyote anayehitaji kuimarisha imani na uwezo wake wa kufanikisha ndoto za maisha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Mikumi, Augustine Masesa, aliitaja Mikumi kama hifadhi inayofikika kwa urahisi kutokana na miundombinu bora.
"Mikumi ni hifadhi inayofikiwa kirahisi kwa sababu ya uwepo wa Treni ya Kisasa ya SGR inayopita Morogoro na barabara ya lami iliyo karibu na hifadhi. Hili linawavutia watalii wa ndani na nje," alisema Masesa.
Mbali na urahisi wa kufikika, Masesa alibainisha ukubwa wa hifadhi hiyo na wingi wa wanyama, akisema: "Mikumi ni eneo linalompa mtalii fursa ya kuona wanyama wengi kwa urahisi, jambo linaloifanya kuwa kivutio cha kipekee."
Aidha, Kamishna Masesa amempongeza mwandishi wa kitabu kwa kutoa kitabu kizuri kinacholenga kusaidia watu kutimiza ndoto zao, pia uamuzi wa kuja kuzindulia hifadhini hapo
Kwa upande wake, Mtemi Renatus Sona, mratibu wa uzinduzi huo kupitia kundi la Shangwe Tour, alieleza sababu za kuchagua hifadhi ya Mikumi kuwa eneo la uzinduzi. "Tulitaka kufanya jambo tofauti. Uzinduzi huu unalenga pia kuhamasisha watu kutembelea hifadhi za taifa na kufurahia vivutio vya asili," alisema Mtemi Sona.
Mhandisi Ronah Mwakisisile, mmoja wa washiriki wa tukio hilo, alikielezea kitabu "Usiishie Njiani" kama mwongozo wa kipekee kwa watu wanaotafuta njia za kufanikisha ndoto zao.
Uzinduzi huo wa kipekee ulihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi wa TBA, TARURA, na wawakilishi wa Hifadhi ya Mikumi, huku ukitoa nafasi ya kipekee kwa wageni kushuhudia uzuri wa wanyama pori usiku.
Mgeni rasmi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Augustine Masesa akikabidhiwa Kitabu Usiishie Njiani na Mwandishi wa Kitabu hicho Eng. Avith Amos.
Mwandishi wa Kitabu, Eng. Avith Amos akisaini Kitabu ambacho alimkabidhi mgeni rasmi kama shukrani ya kuzindua kitabu hicho!
0 Comments