Ticker

6/recent/ticker-posts

Prof. Mkenda: Uwekezaji katika Sayansi na Teknolojia Ni Muhimu kwa Maendeleo Endelevu ya Tanzania

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Tanzania inahitaji kuongeza uwekezaji katika sayansi na teknolojia ili kuwa na rasilimali watu mahiri wenye uwezo wa kuendeleza rasilimali zilizopo nchini.

‎Amesema bila kuwekeza katika maeneo hayo, watakwama na badala yake, rasilimali asili zitakuwa laana na si baraka.

‎Akifunga Kongamano na maonyesho ya tisa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jana Dar es Salaam, Profesa Mkenda alisema nchi zilizoendelea zina maendeleo endelevu kwa sababu ya kujenga rasilimali watu kama mtaji hivyo ni lazima kuwekeza kwenye elimu.

‎"Tunazo rasilimali za asili za kutosha nchini kama vile madini, lakini tusipokuwa na uwezo wa kuzichakata na kuwaachia watu kutoka nje, tutakwama," alieleza.

‎Profesa Mkenda alisema wanahitaji sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati kuendelezwa ili kuwa na vijana mahiri katika maeneo hayo watakaoweza kuchangia katika maendeleo ya uchumi.

‎Alisema wataendelea kuongeza jitihada ya kuwekeza katika sayansi na teknolojia sambamba na kusomesha vijana kwenda nje ya nchi kuongeza umahiri.

‎"Tunatoa mikopo kwa upendeleo wa wanafunzi wa sayansi lakini hatupaswi kuchoka ili elimu iwe bora zaidi na kuzingatia sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu vijana wawe mahiri katika maeneo hayo," alisisitiza.

‎Pia alisema kwa kufanya hivyo, watatoa vijana wabobevu watakaosaidia katika maendeleo na kwamba watawaunganisha na maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo viwandani kuongeza ujuzi.

‎Kuhusu Mfuko wa Ubunifu wa Samia, Profesa Mkenda alisema kuwa umelenga kuwezesha wabunifu kubiasharisha bunifu zao badala ya kuendelea kushiriki kwenye maonesho.

‎Alisema sababu ya kuanzishwa kwa mfuko huo ni benki kushindwa kukopesha wabunifu kwa madai kwamba hawakopesheki na kwamba ni bunifu zinazoanza ziko katika hatari.

‎"Mfuko wa Ubunifu una zaidi ya Sh bilioni 6 ni mtaji kwa wabunifu waweze kuuza bunifu zao. Tunataka bunifu mpya na sio zilezile kila mwaka," alieleza Profesa Mkenda.

‎Pia alisema mfuko huo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuna fedha kwa watafiti, wabunifu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masono ya Sayansi, teknolojia na ubunifu.

‎Alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya utafiti wa mabadiliko ya tabia nchi ili kuona namna ya kukabiliana nayo.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu alisema mada mbalimbali ziliwasilishwa kwenye kongamano hilo la siku tatu na mapendekezo yaliyotolewa ni kuimarisha midahalo ya wadau, kutekeleza sera ya viwanda kwa kushughulikia changamoto za sera hiyo na kuunganisha ushirikiano kati ya elimu ya juu na viwanda pamoja na kuunganisha sekta ya viwanda, sayansi na teknolojia.

‎‎Alisema kuna mapendekezo ya kuwa na teknolojia zitakazowasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

‎"Costech imeombwa iratibu nyenzo au vifaa vya utafiti vitakavyotumiwa kwa pamoja na watafiti kutokana na gharama za juu za vifaa hivi, pia imeshauriwa kuwekeza teknolojia zenye gharama nafuu kuondoa hewa ukaa," alisema Dk Nungu.

‎Pia imeshauriwa watafiti wajikite kufanya utafiti uchumi wa kibaolojia.

‎Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi alisema nchi inahitaji maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu yaweze kuimarishwa ili kukuza uchumi.

‎Alisema mijadala iliyojadiliwa kwenye kongamano hilo, ilijikita maeneo matano ikiwemo matumizi ya maarifa asilia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, uendelevu usalama wa chakula na kukuza sayansi, teknolojia na hisabati kwa uchumi stahimilivu na kuendeleza uchumi wa buluu wanahitaji wataalamu mahili kushika eneo hilo.

‎"Tutashirikiana kutekeleza maazimio haya kwa kushirikiana kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na kuweka utaratibu sahihi ili kutekeleza maazimio hayo na kupiga hatua.

Post a Comment

0 Comments