Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA); kuanzia tarehe 20 Januari, 2025 itaanza kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 mkoani Singida ili kusaidia Wananchi kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.
Hayo yamesemwa leo, tarehe 22 Desemba, 2024 na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Bi Martha Chassama Kutoka REA akimuwakilishi Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy mbele ya wananchi wa Kijiji cha Kideka Wilayani Ikungi.
Katika mpango huo; Mkoa wa Singida unataraji kupokea mitungi ya gesi 19,530 yenye thamani ya shilingi milioni 406.7 ambayo, itasambazwa kwa Wananchi katika wilaya zote sita huku kampuni ya Lake Gas ikipewa jukumu la kusambaza mitungi hiyo kwa gharama ya shilingi 20,825 kwa kila mtungi (Bei ya ruzuku).
Imeelezwa kuwa Serikali, itatoa ruzuku ya asilimia 50 kwenye kila mitungi ambapo bei ya awali, ilipaswa kuwa shilingi 41,650 ili kununua mtungi pamoja na kichomeo chake.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Mhe Martha Gwau amepongeza juhudi hizo za Serikali na kuongeza kuwa lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, jambo ambalo litasaidia kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Serikali, imeweka ruzuku ya asilimia 50, kwa hiyo wakina Baba na kina Mama wa mkoa wa Singida, wajiandae kutumia gesi, tuwapunguzie wakina Mama kushika masizi, kutumia kuni na mikaa, kwetu sisi Mradi huu ni neema”. Alisema, Mhe Gwau
Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuasisi mpango huo wa nishati safi kwa wanachi huku akitoa ruzuku kwa wananchi kwa ajili ya kwenda sambamba na mpango huo wa serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ikungi Ndg Mika Likapakapa amesema kuwa mradi huo unaimarisha matakwa na utekelezaji wa ilani ya CCM kama ambavyo imeainisha kuimarisha sekta ya nishati kuwa na nishati safi ya kupikia sambamba na kuhifadhi mazingira ya Tanzania.
Bi, Chassama amesema ili kupata mtungi huo wenye ruzuku ya Serikali kila Mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA.
Amesema, REA pia imegawa mitungi 100 kwa wananchi ambao ni wajasiriamali katika kijiji cha Kideka Wilayani Ikungi ikiwa imeitikia ombi la mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Singida Mhe Martha Gwau.
0 Comments