Ticker

6/recent/ticker-posts

TASAF WAKAMILISHA UJENZI NYUMBA ZA WATUMISHI ZAHANATI MDUNDUWALO, WANANCHI WAISHUKURU SERIKALI

Na Said Mwishehe,Songea

WANANCHI wa Kijiji cha Mdunduwalo kilichopo Kata ya Peramiho wilayani Songea Mkoani Ruvuma wameushukuru Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF)kwa kukamilisha Ujenzi wa nyumba za watumishi wa Zahanati ya Mdunduwalo.

Wamesema kukamilika kwa nyumba za watumishi wa zahanati hizo umewezesha kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya kwani wauguzi na Madaktari wamekuwa Karibu na eneo la kutoa huduma za afya kwani kabla ya Ujenzi wa nyumba watumishi hao walikuwa wakaa mbali na zahanati, hivyo kufanya upatikanaji wa huduma za afya kuzipata kwa shida.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo leo Desemba 19,2024 wananchi hao wamesema kukamilika kwa nyumba za watumishi kumefanya wawe na uhakika wa matibabu iwe mchana au usiku na kubwa zaidi kwa gharama nafuu kwani hakuna gharama ya nauli ya kumfuta Muuguzi au daktari Peramiho kwani sasa wanapatikana hapo hapo.

Mkazi wa Kijiji cha Mdunduwalo ambaye pia ni Mzimamizi wa Zahanati hiyo Agustino Luhwoga huduma katika zahanati hiyo ilikuwa inatolewa kwa masaa, na kuna wakati watoa huduma wanakuwa hawapo hasa wakati wa mwishoni mwa wiki wahudumu wa afya wanakuwa hawapo

Ameongeza kuwa wahudumu wengi walikuwa wanakaa mbali,hivyo ilikuwa inatulazimu kusafiri kutoka kijijini hapa kwenda Peramiho mjini au Songea kufuata huduma za afya au kuwakodia usafiri wahudumu wa zahati kwa ajili ya kupata huduma za afya lakini uamuzi wa TASAF kujenga nyumba za watumishi umeondoa changamoto zilizokuwepo kwa wanakijiji.

“Baadhi ya wagonjwa walikuwa wanapoteza maisha wakiwa njiani kufuata huduma, lakini kwa sasa watoa huduma wapo hapa hatuna haja ya kusafiri kwenda mbali, tunashukuru kwa kukamilika kwa ujenzi wa miradi hii ya nyumba za wauguzi na waganga.” Amesema.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji hicho, Zawadi Mlapone, amesema kwamba mradi wa ujenzi wa nyumba hizo, kisima cha maji na matundu nane ya vyoo umeendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwenye zahanati hiyo.

Amefafanua kabla ya kupata nyumba ya waganga wananchi walikuwa wanapata shida ya kupata huduma za afya hasa nyakati za usiku lakini tangu wamepata nyumba wananchi wanapata huduma.Pia wanashukuru kwa kupata kisima cha maji ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuleta huduma kwetu lakini tunawashukuru TASAF kwa kutekeleza miradi hii hapa Kijijini kwetu.Wananchi tunashukuru sana na ombi letu kubwa kwa Serikali na TASAF tusaidiwe gari ya wagonjwa,"amesema na kuongeza huduma katika zahanati hiyo zimeanza Aprili mwaka jana lakini watumishi walikuwa wanakaa mbali kwa kukosa nyumba .

Awali Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea, Ahosana Ngunge ameeleza kwamba mradi huo ulianza mwaka jana baada ya kuombwa na wananchi na kukamilika Machi mwaka huu.

"Mradi huu umeghalimu shilingi milioni 179 ambazo zimetumika kujenga nyumba mbili za wafanyakazi wa kituo, matundu nane ya vyoo, kuchimba kisima pamoja na ujenzi wa kichomea taka," alisema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mwalimu Hassan Mtamba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais DK.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia miradi ya TASAF inayotekelezwa katika halmashauri yao ukiwemo mradi wa stendi ya mabasi na zahanati inayojengwa Mdundwaro na kwa ujumla miradi inaendelea vizuri.

"Mradi wa zahanati utaondoa adha ya wananchi kupata huduma za afya lakini mradi wa stendi pia utaondoa adha ya wananchi mbalimbali pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika kupata usafiri .Miradi yote inaendelea vizuri na tunaamini italeta tija kwa wananchi.

"Serikali inaimani kubwa sana na sisi tunatekeleza miradi lakini tunaomba na wananchi waendelee kuwa na Imani na Serikali yao kwasababu inalengo nzuri la kuendelea kuwasogezea huduma karibu.Watumishi wa Serikali tutaendelea kusimamia miradi na kusimamia vema fedha za serikali kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Nyumba ya wafanyakazi wa Zahanati ya Mdundwaro katika kijiji cha Mdundwaro kata ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ikiwa imekamilika.
Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea, Hosana Ngunge (kushoto) akimuonyesha muuguzi wa  Zahanati ya Mdundwaro,  Sinasudi William alama ya uzinduzi wa ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Zahanati hiyo.

Post a Comment

0 Comments