NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WASHIRIKI wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wamepitia rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo Serikali ilitoa hivi karibuni na kuangalia mapungufu ya kijinsia na kutoa mapendekezo yao.
Akizungumza katika semina hizo Januari 15 ,2025 katika viwanja vya TGNP-Mtandao Jijini Dar es Salaam, Mwezeshaji wa Mada, Deogratius Temba amesema wakipata muda wa kukutana na Kamati ya kukusanya maoni watawapa mapendekezo ya maboresho ya baadhi ya maeneo machache ambayo walitegemea yangekuwepo.
“Baada ya kupokelewa mapendekezo, tunaamini Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 itakuwa imakamilika ambayo imebeba sauti za watu wote wakiwemo wananchi walioko pembezoni hasa wakulima, wafugaji na watu wenye ulemavu.
Aidha amesema masuala ya ukatili wa kijinsia yanetajwa lakini hayajawekewa mikakati ya kutokomeza au kuzuia.
Pamoja na hayo amesema suala la bajeti lenye mlengo wa kijinsia pia halijazungumzwa kwani wangetamani yangetajwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Miburani, Vivian Lugulumu amesema licha ya vitu vingi kupendekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, wanatamani waoneshwe mkakati wa kuweza kufanya kazi katika masuala yote ya kimaendeleo yaliyooanishwa.
“Suala la afya limejielezea vizuri kabisa kwamba tutapata huduma bora za afya lakini kuna mapendekezo sisi tulipenda yaainishwe, kwa mfano, masuala ya mama mjamzito,wazee na watoto waliochini ya miaka mitano bado hayajawekwa wazi kama watapata huduma bure au watalipia”. Amesema Vivian.
Nae Mshiriki wa GDSS, Shiganga George amesema kwenye Dira haijaonesha moja kwa moja kwamba itasaidia kwa kiasi gani wanafunzi wa kike ambao wapo kwenye hedhi.
0 Comments