Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KOMBO AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA MAGHARIBI B

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesema kuimarika kwa miundombinu ya Mahakama ni hatua muhimu itakayowawezesha wananchi kupata huduma katika mazingira mazuri, salama na rafiki.

Ameyasema hayo leo Januari 1, 2025 wakati akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B huko Kisakasaka, Zanzibar.

Balozi Kombo amesema, kwa miaka mingi mahakama zimekuwa na changamoto ya miundombinu ya majengo na Serikali inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kumaliza changamoto hizo kwa kujenga majengo mapya na ya kisasa.

"Kwa mfano jengo lililokuwa likitumiwa na Mahakama ya Magharibi B pale Mwanakwerekwe lilikuwa finyu mno kiasi cha kusababisha msongamano mkubwa na kuwapa usumbufu waliofuata huduma mahali pale," alisema Mhe. Kombo.

Waziri huyo ameongeza kuwa, pamoja na ufinyu huo, pia halikuwa rafiki kutokana na kukosekana nafasi kwa ajili ya maofisa wa Mahakama.

Vilevile, kukosekana kwa huduma za watu wenye mahitaji maalumu na maegesho kulisababisha muda mwingi wananchi walikuwa wanazagaa kwa kukosa sehemu tulivu ya kusubiri huduma.

Amesema, hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuchukua hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya mikoa na wilaya Unguja na Pemba.

Pia, amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Kwa upande wa Unguja, Balozi Kombo amesema, mradi huo wa Loti Nambari 2 unajumuisha majengo manne ambayo ni: Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mahakama ya Mkoa wa Kusini na Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B.

Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya majengo ya ofisi, hivyo ni wajibu wa watumiaji wa miundombinu hii na wananchi kwa ujumla kuitunza ili iweze kudumu kwa miaka mingi ijayo.

Post a Comment

0 Comments